LOGO

LOGO

Saturday 30 May 2015

Kiafya zaidi!

Hasira inaathiri afya na ubora wa maisha!
Hasira ni hali ambayo mara nyingi humpata binadamu na wanyama wengine katika kipindi cha maisha yao.
Hasira ni mwitiko wa mwili dhidi ya hisia za tishio la kutambulika,usalama,ustawi,mamlaka,sifa, heshima au mafanikio ya mtu.
Hasira ni kengele ya mwili inayoashiria kuwa kuna jambo Fulani haliendi kama tunavyofurahia na kulitazamia liwe au haki haikutendeka.
Wakati mwingine mambo yanayowafurahisha wengine yanaweza kusababisha hasira kwa watu wengine na kuleta mgongano wa masilahi.

Jambo la kushangaza ni kwamba wakati Fulani hasira husababishwa na mahusiano kati yetu na watu tunaowapenda sana.
Kwa maana hiyo hasira huwa kama onyo kwa watu wengine kuhusu mambo ambayo hayatufurahishi katika mahusiano. Katika hali kama hiyo hasira iliyodhibitiwa vizuri,inaweza kuwa faida kwa ajili ya kudumisha mahusiano.

Baadhi ya ya wachunguzi wa maisha ya binadamu wanaamini kuwa hasira ni sehemu ya maumbile yetu na kwamba binadamu asiye na hasira ana upungufu.

Taasisi ya ya anger research consortium ya chuo kikuu cha southern mississipi na chuo kikuu cha Wisconsin-green bay inayojihusisha na utafiti wa hasira inasema kwamba,watu wengi sana hupata hisia ndogo za kukasirisha mara chache ndani cha juma moja.

Katika utafiti huo, inaaminika kuwa theluthi moja sawa na asilimia 33 ya watu wote hupata hasira kali kila siku.
Watu hukasirishwa na mambo tofauti kutegemea na umri,jinsi,mila na hata utamaduni wao. Lakini pia watu huwa na mwitikio tofauti wanapopandwa na hasira.

Baadhi ya watu hawakasiriki upesi na husahau haraka wanapokosewa, lakini wengine hukasirika kwa muda wa siku, majuma, miezi au hata miaka kadhaa.

Waswahili kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiamini kuwa hasira ni hasara, lakini wanasayansi wanasema kuwa pamoja hasara,hasira inaweza kuwa na faida kadhaa katika hali Fulani za maisha.
Kaika utafiti  uliofanywa na shinobu kitayama wa chuo kikuuu cha Michigan na wenzake ilinainika kuwa baadhi ya jamii kama vile wajapani, kuonyesha kiwango Fulani cha hasira huimarisha afya za mwili na hisia.

Wanasanyansi wanasema katika maisha ya kawaida ya binadamu si rahisi kuepuka hasira. Jambo la muhimu ni kuelewa jinsi ya kutawala hasira ili isisababishe madhara ya kiafya na mahusiano ya kijamii.

ATHARI ZA HASIRA.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hasira kali isiyodhibitiwa inadhuru afya ya mwili na akili pia.
Profesa Herbet benson, raisi mwanzilishi wa taasisi ya uhusian wa afya ya akili na mwili wa Harvard anasema kuwa mlipuko wa hasira kali si jambo jema kwa afya.

Dk.Dan E.Shoultz, mwanasaikolojia katika kituo cha ushauri(PCA) nchini marekani anasema: "Mungu ametuumba kwa namna ambayo hatupaswi kuwa na hasira kwa muda mrefu....tunapofanya hivyo tunajiumiza wenyewe na hali hii husababisha kuharibika taratibu kwa mfumo mzima wa mwili."

 Hasira kali isiyodhibitiwa inaweza kusababisha magonjwa kama vile kiharusi,shambulio la moyo la ghafla, maumivu ya kichwa, maumivu ya tumbo, vidonda vya tumbo, kukosa usingizi, wasiwasi, shinikizo la damu.

Madhara mengine ya hasira kali ni utendaji mbaya wa figo, msongo wa mawazo, upungufu wa kinga mwilini na maumivu ya mwili bila sababu bayana.

Kwa mujibu wa utafiti wa Jean-Philippe Gouin na wenzake uliochapishwa katika jarida la sayansi za tiba lijulikanalo kwa jina la Brain,behaviour and immunity toleo la Desemba 8,2007, hasira isipodhibitiwa inachelewesha na uponyaji wa vidonda.

Hasira kali zisizodhibitiwa pia husababisha madhara kwa wengine katika jamii. Wananchi wenye hasira kali hujichukulia sharia mikononi na kupoteza maisha ya watu wengine wakati mwingine bila ya kuwa na hatia.

Hasira kali hasa kwa madereva pia ni moja ya vyanzo vya ajali za barabarani zinazopoteza afya na maisha ya watu wengi.

Uchunguzi unaonyesha pia kina mama wajawazito wanaoshindwa kudhibiti hasira zao, pia huwaathiri watoto wao ambao hawajazaliwa.

Mara nyingi binadamu hukasirika pale anapopata hisia za kweli au zisizo za kweli juu ya jambo baya dhidi yake, jamii ama maslahi yanayomuhusu.

Baadhi ya tafiti zinasema kwamba watu wanaoshindwa kudhibiti hasira zao hadi kufikia hatua ya  kusababisha madhara ya kiafya kwao na kwa wengine.

Wasio na udhibiti wana matatizo ya afya ya akili katika sehemu ya ubongo inayojishughulisha na usimamiaji wa hisia za mwili katika sehemu ya mbele ya ubongo inayoshughulika na mfumo wa uamuzi.

:Kwa hisani ya Clifford Majani,Mwananchi: